Boko Haram wametimua watoto nusu milioni
- sembula
- Sep 19, 2015
- 1 min read

Watoto nusu milioni wametoroka makwao kutokana na mashambulio ya kundi la wapiganaji wa Kiislamu la Boko Haram katika kipindi cha miezi mitano iliyopita, shirika la UN linalowashughulikia watoto limesema.
Unicef inasema idadi hiyo inafikisha jumla ya watoto waliotoroka mashambulio ya kundi hilo Nigeria na mataifa jirani hadi 1.4m.
Maelfu ya watoto wameathiriwa na utapiamlo na baadhi ya kambi zimekumbwa na kipindupindu.
Mashambulio ya Boko Haram yameongezeka baada ya wapiganaji hao kufurushwa kutoka kwa maeneo mengi waliyodhibiti kupitia operesheni ya pamoja ya mataifa yaliyoathiriwa na mashambulio ya wanamgambo hao.
"Nigeria kaskazini pekee, watoto karibu 1.2m, zaidi ya nusu yao wakiwa na umri wa chini ya miaka mitano, wamelazimika kutoroka makwao,” Unicef ilisema kupitia taarifa.
Watoto wengine 265,000 wamehama makwao Cameroon, Chad na Niger, ripoti hiyo imesema.
Comments