top of page

Wahamiaji 1000 wawasili Ujerumani

  • Writer: sembula
    sembula
  • Sep 1, 2015
  • 2 min read

Treni zinazobeba mamia ya wahamiaji zimewasili katika mji wa Munich nchini Ujerumani, baada ya Hungary kusitisha juhudi zake za kuwasajili chini ya sheria za Muungano wa Ulaya.

Wahamiaji 1,400 waliwasili mjini Munich mapema hii leo, baada ya kupitia Austria na wahamiaji wengine wengi zaidi wanatarajiwa kuwasili.

Polisi nchini Hungary sasa wamefunga kituo kikuu cha treni mjini Budapest katika juhudi za kudhibiti mzozo huo.

Idadi ya wahamiaji wanaowasili barani Ulaya imefikia rekodi ya juu zaidi kuwahi kunakiliwa.

Mwezi Julai mwaka huu pekee wahamiaji 107,500 waliwasili barani Ulaya.

Image copyrightEPA

Image captionWahamiaji wakiwa nje ya kituo cha treni cha Keleti mjini Budapest

Nje ya kituo cha Keleti kilichoko Mashariki mwa Budapest, takriban wahamiaji 1,000 wamekuwa wakiimba "Ujerumani, Ujerumani", wakitaka kituo hicho kifunguliwe ndipo waendelee na safari yao.

Ujerumani inatarajia kuwapokea wahamiaji 800,000 mwaka huu kiwango ambacho ni mara nne jumla ya wahamiaji iliopokea mwaka jana.

Wengi wa waliosafiri Munich, walikaa kituo cha Keleti siku nyingi na waliabiri treni za kwenda Vienna hiyo jana, polisi walipoonekana kukata tamaa kuwasajili.

Wanahabari walisema wengi wa wahamiaji hao wametoka Syria, Afghanistan na Eritrea.

Maafisa Austria, wanasema 3,650 waliwasili kwa treni mjini Vienna siku ya Jumatatu.

Image captionRaia wa Austria wakiandamana kupinga wahamiaji

Wengi wanataka kwenda Ujerumani.

Chini ya Kanuni za Dublin za Muungano wa Ulaya, EU, wanaotafuta hifadhi ni sharti wajiandikishe katika taifa la kwanza mwanachama wa EU wanalotua.

Hata hivyo, sheria hizo zimekuwa zikikiukwa, kwani wengi wa waliofika Hungary mwanzo walitua Ugiriki, ambako walishindwa kudai hifadhi.

Serikali ya Berlin tayari imesema inasimamisha utekelezwaji wa kanuni hizo za Dublin, kwa Wasyria waliofika Ujerumani.

Chansela Angela Merkel, mnamo siku ya Jumatatu aliitisha kuwepo kwa ushirikiano zaidi miongoni mwa wanachama wa EU kuhusu suala hilo na bila kusema waziwazi akatoa wito kwa mataifa mengine kupokea wakimbizi zaidi.

Image captionChansela wa Ujerumani Angela Merkel na viongozi wengine wa Uaya

Huku idadi ya wahamiaji wanaopitia Hungary ikiendelea kuongezeka, Austria imejaribu kuweka vizuizi zaidi vya kuchunguza magari yanayovuka mpaka.

Hatari wanazokumbana nazo wahamiaji zilionekana wazi wiki iliyopita wakati wahamiaji 71 walipopatikana wamefariki ndani ya lori walilokuwa wakisafiria kutoka Budapest kwenda Austria.

Wengi wa waliofariki wanakisiwa kuwa Wasyria wanaotoroka vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini mwao.

Watu wanaokadiriwa kuwa 20,000 waliandamana nje ya majengo ya bunge mjini Vienna siku ya Jumatatu wakiitisha kuwepo kwa haki zaidi kwa wahamiaji.

Kando na miili iliyopatikana kwenye lori Austria, mamia ya watu walikufa maji katika bahari ya Mediterranean wiki iliyopita wakijaribu kufika bara Ulaya kutoka Libya.


 
 
 

Comments


RECENT POSTS:
SEARCH BY TAGS:

© 2023 by NOMAD ON THE ROAD. Proudly created with Wix.com

  • b-facebook
  • Twitter Round
  • Instagram Black Round
bottom of page